Na Nova Kambota,
Jumatano, 26 June 2013
“Unless not later than 11 a.m , British summer time , today September 3rd ,satisfactory assurances have been given by the German government and have reached His Majesty’s Government in London, a state of war will exist between the two countries from that hour”
Hivi ndivyo ujumbe wa serikali ya Uingereza kwenda kwa Adolf Hitler ulivyosomeka siku ya tarehe 3 septemba 1939, masaa machache baadae ulimwengu ukaingia katika kile kilichokuja kujulikana kama vita kuu ya pili ya dunia (1939-1945) ambayo inaelezwa kuwa mpaka leo hii vita hiyo imevunja rekodi ya dunia kwa kuwa vita iliyoteketeza roho za watu wengi zaidi tangu dunia ilipoumbwa.
Tatizo kubwa ambalo wanahistoria wengi wanalifanya ni kujadili janga hili (vita kuu ya pili ya dunia) kwa mtizamo finyu ambao mwisho wake huwa ni kurusha lawama za upande mmoja kwa kumlaumu Adolf Hitler pekee! Kwasababu za kitaaluma, uchambuzi na historia makala hii inajaribu kuibua fikra mpya kwa kutanua mjadala wa nani mwenye kubeba lawama kwa vita hii? Nifate katika makala hii ya kusisimua ambayo itapanua uwezo wako wa kujenga hoja ……………..
Wakati Adolf Hitler anaingia madarakani mwaka 1933 tangu miaka ya mwanzoni ya utawala wake Hitler alionyesha msimamo mkali dhidi ya mkataba wa amani wa Versailles(Versailles Peace Treaty) ambao ulitiwa saini mwaka 1919 kati ya mataifa yaliyoshinda vita kuu ya kwanza ya dunia, kimsingi mkataba huo “uliinyonga” ujerumani kwa kigezo cha kuwa “mwanzilishi” wa vita kuu ya kwanza ya dunia. Hitler alipokuwa kiongozi wa Ujerumani alipingana vikali tena waziwazi na mkataba huu lakini si Uingereza wala Ufaransa waliojitokeza kumpinga Hitler, kwanini?
Ukweli wa mambo ni kuwa licha ya makataba wa amani wa Versailles kutiwa saini lakini kwa nchi nyingi ulitafsirika kuwa si wa amani bali wa kisasi dhidi ya Ujerumani, vyanzo mbalimbali vinathibitisha kuwa hata wakati Hitler alipoanza “ukorofi” wake baada ya kutwaa madaraka nchini Ujerumani wanasiasa wakubwa wa nchini Uingereza akiwemo Neville Chambarlain waliona masharti mengine ndani ya mkataba wa Versailles yalikuwa hayatekelezeki, kwa maana nyingine walibariki uamuzi wa Hitler kukiuka baadhi ya masharti haya.
Sera hii ya kumwacha Hitler kama siyo kumridhisha iliasisiwa na Neville Chamberlain na baadaye kuungwa mkono na Ufaransa ilikuja kujulikana kama “Appeasement Policy” ambayo kimsingi ililenga “kumridhisha” Adolf Hitler na “kuwafariji” Wajerumani kwa kile kilichoonekana kuwa walionewa sana na mkataba wa Versailles. Akiunga mkono sera hiyo ya “kumpoza” Hitler na wajerumani mwenyewe Chambarlain ananukuliwa akisema “If only we could sit down at a table with the Germans and run through all their complaints and claims with a pencil, this would greatly relieve all tension” haya ndiyo yalikuwa mawazo ya waziri mkuu wa Uingereza.
Kuzaliwa kwa sera ya Appeasement siasa za kidezodezo , mwenendo wa kumwacha Hitler kufanya “lolote” ndiko kwa kiwango kikubwa kulikosababisha kuibuka kwa vita kuu ya pili ya dunia 1939. Mataifa yaliyobuni na kutekeleza sera hii ya “kipuuzi” ama “busara” si mengine bali ni Uingereza na Ufaransa. Je kwa kuzingatia hili ni sahihi kumlaumu Hitler pekee? Kwanini Uingereza na Ufaransa zinasafishwa kutoka dhambi hii?
Ni vema ikaeleweka kuwa wanahistoria wote wanakubaliana kuwa Appeasement Policy ilichangia kwa kiasi kikubwa kuibuka kwa vita kuu ya pili ya dunia, tofauti ni kuhusu mantiki ya sera hii, swala la uhalali au uharamu wa sera hii ni lingine isipokuwa la muhimu ni kuwa chimbuko la vita kuu ya pili ya dunia ni sera ya Appeasement ya Uingereza na Ufaransa.
Kwanini Appeasement Policy ni halali?
Miaka ya karibuni kumeibuka kundi la wanahistoria wa kizazi kipya hususani nchini Uingereza ambao wanajaribu kwa kiasi kikubwa kuitetea “Appeasement Policy” kwa nguvu kubwa lengo likiwa ni kulinda heshima ya Neville Chambarlain. Watetezi hawa wanatoa hoja zifuatazo;
(i)Faraja kwa Ujerumani
Mwanzoni viongozi wengi wa dunia wa wakati ule akiwemo Chambarlain wa Uingereza pamoja naye Daladier wa Ufaransa waliamini kuwa kwa kiasi Fulani madai ya Hitler na Wajerumani yana mantiki, ni madai halali kwa kuzingatia ukweli kuwa mkataba wa Versailles uliadhibu vibaya sana Ujerumani, kwa hiyo kila hatua ambayo Hitler alichukua mara moja ilihalalishwa na Uingereza na Ufaransa kwa matumaini kuwa Hitler ataridhika na kutulia.
(ii) Lengo la kuwa na amani ya kudumu
Ni ukweli usiopingika kuwa Uingereza na Ufaransa walihitaji amani ya kudumu barani ulaya, kumbukumbu za mapigano ya vita kuu ya kwanza ya dunia zilikuwa zingali mbichi kwa mataifa haya ya kibeberu, Chambarlain na Daladier kwa pamoja waliamua kumridhisha Hitler kwa kumkubalia yale aliyotaka ilikuwa njia mwafaka ya kumfanya atulie hivyo kuleta amani.
(iii) Hofu ya Ukomunisti
Kwa sababu za kiusalama Uingereza na Ufaransa walihofia kuenea kwa ukomunisti katika nchi za Ulaya ya Mashariki ikiwa watamtumia Joseph Stalin kupenyeza utawala wao katika upande huo wa Ulaya badala yake wakaamua kumtumia Hitler kudhoofisha kuenea kwa ukomunisti katika mataifa ya Poland na Czechoslovakia, kwa kumwacha Hitler(adui mkubwa wa ukomunisti) madarakani kulihakikisha kuwa ukomunisti haupenyi na kusambaa Ulaya ya Mashariki, hii ndiyo sababu Uingereza na Ufaransa hazikutaka kumghasi Adolf Hitler.
(iv)Muda wa kuimarisha majeshi (time to re-arm)
Hoja kubwa inayotumika kuhalalisha Appeasement policy ni kuwa Uingereza haikuwa tayari kwa vita. Mkakati wa kuiandaa Uingereza kwa vita ulianza mwaka 1936 na ulipangwa kumalizika mwaka 1940, ndiyo maana katika mgogoro uliopelekea mkataba wa Munich wa mwaka 1938 Chamberlain alikubaliana na matakwa ya Hitler, kwa kufanya hivyo vita iliahirishwa kwa mwaka mzima kabla ya kulipuka hapo 1939 wakati Uingereza ilikwisha jiandaa vya kutosha( When the crises of 1938 occurred, Britain desperately needed more time to build up its strength. By giving into Hitler’s demands at Munich, war was postponed for a year, and when it did eventually come, Britain had made just enough preparations to survive).
Kwanini Appeasement Policy ni haramu?
Mwezi oktoba 1938, aliyekuwa kiongozi wa chama cha Labour cha Uingereza Clement Attlee alinukuliwa akisema “the events of the last few days are one of the greatest diplomatic defeats this country and France have ever suffered. There can be no doubt that it is a tremendous victory for Herr Hitler. Without firing a shot, he has achieved a dominating position in Europe” hapa ilikuwa baada ya mkataba wa Munich ambapo Chambarlain na Daladier walimruhusu Hitler kuivamia na kuiteka Czechoslavakia nchi iliyokuwa inainukia kiuchumi barani Ulaya.
Ambalo la msingi kuzingatia ni kuwa baada ya mkutano wa Munich si Chambarlain wala Daladier walioamini kuwa wamefanya jambo sahihi kumruhusu Hitler kuivamia Czechoslovakia, wote hawakuliamini hili hata kama kwa kuwapotosha waingereza Chambarlain ananukuliwa akisisitiza kwa kusema “I believe it is peace for our time” naye Daladier alipofika uwanja wa ndege wa Paris kinyume na matarajio yake wafaransa walimpokea kwa shangwe kwasababu walishaleweshwa na propaganda naye kwa kutambua ukweli huo aliishia kuwaita wajinga “at the airport Daladier turned up his coat collar to protect his face from the rotten eggs he expected from the crowd. To his astonishment there were no eggs or shouts of ‘We are betrayed’. Instead they were actually cheering him-shouting ‘Vive Daladier ‘ , ‘ Vive la Paix ‘ , Vive la France!’ Daladier turned to a collegue and whispered, ‘The fools!’ . Hapa jambo la kuzingatia ni kuwa hata viongozi wa Uingereza na Ufaransa wenyewe waliona wamekosea, wamekosea kwa sera yao ya Appeasement, sera hii ilikuwa haramu kwa kuzingatia hoja hizi;
(i)Uingereza na Ufaransa hawakumwelewa Hitler kiundani(The appeasers misjudged Hitler)
Chambarlain na Daladier walifanya kosa kubwa sana la kumchukulia Hitler kama mwanasiasa makini mwenye uwezo wa kutambua mema na mabaya na ambaye alikuwa tayari kujadiliana. Hawakumwelewa Hitler mpaka walipojikuta wamekwishachelewa sana, baadae sana walikuja kutambua kuwa walikuwa wanacheza na dikteta hatari ambaye kila walipojishusha na kumkubalia matakwa yake yeye alitafsiri kuwa ni udhaifu, kadri walivyompa ndivyo alivyohitaji zaidi(The more they gave him , the more he demanded).
(ii)Appeasement ilikuwa na udhaifu wa kimantiki
Uingereza na Ufaransa walihofia sana vita nyingine kiasi cha kuiruhusu Ujerumani kuvunja makubaliano ya kimataifa pasipo adhabu yoyote, mwishowe waliacha Hitler kuivamia Czechoslovakia kwa ahadi hewa zisizo na maana yoyote. Sera ya Appeasement haina maneno mengine ya kuielezea isipokuwa udhaifu na uoga(Appeasement was simply another word for weakness and cowardice).
(iii) Uingereza na Ufaransa zilishindwa kutumia vizuri fursa za kumzuia Hitler
Uingereza na Ufaransa kwa pamoja walipoteza muda mwingi kuridhia matakwa ya Hitler kiasi cha kushindwa kutumia fursa nyingi za kumzuia zilizojitokeza. Mfano Adolf Hitler mwenyewe ana kiri kuwa ikiwa Ufaransa na Uingereza wangezuia mpango wake wa kuimarisha jeshi lake katika eneo la Rhineland mwaka 1936, basi asingekuwa na mbadala zaidi ya kuachana na mpango huo lakini kwa bahati mbaya Uingereza na Ufaransa walifumba macho na kumwacha Hitler aendelee na vurugu zake kwa maana nyingine walitumia sera dhaifu ya Appeasement. Uingereza na Ufaransa walitumia muda mwingi kungoja kusikiliza Hitler atadai nini ili wampe badala ya kuandaa mikakati ya kumzuia kuvunja makubaliano ya kimataifa.
Uingereza na Ufaransa wana dhambi ya kubeba!
Ikiwa Uingereza na Ufaransa walibuni na kutekeleza Appeasement Policy kwa lengo la kuzuia vita isitokee huku wakijua wazi kuwa Hitler hakuwa mtu wa kutosheka hata kidogo, je kwanini mataifa haya yasibebe lawama? Mara baada ya kuzuka kwa vita kuu ya pili ya dunia 1939 Chambarlain anakaririwa akisisitiza “This is a sad day for all of us, and to none is sadder than to me. Everything that I have worked for, everything that I have belived in during my public life, has crashed into ruins” hii ndiyo kauli ya Neville Chambarlain kiongozi wa Uingereza aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuitumbukiza dunia katika vita kuu ya pili ya dunia sambamba na Ufaransa .
Ni ngumu kueleza chimbuko la vita kuu ya pili ya dunia pasipo kuihusisha Uingereza na Ufaransa, si sahihi kuchambua uovu wa Adolf Hitler bila kumhusisha Chambarlain na Daladier! Kwa kutambua kabisa Uingereza na Ufaransa “walilea” tatizo ambalo liliitumbukiza dunia kwenye janga la vita, Adolf Hitler ni mwovu kweli ,ni mhanga wa kihistoria , ni zao la sera dhaifu za Uingereza na Ufaransa ambazo pasi na shaka hazina budi kugawana zigo la lawama na Ujerumani kwa kusababisha vita kuu ya pili ya dunia 1939-1945, pasipo ubishi wowote Uingereza na Ufaransa kwa pamoja zinapaswa kuibeba dhambi hii ya kihistoria.